Kikosi cha soka cha Bungoma Superstars kilijihakikishia nafasi ya kusalia katika ligi kuu nchini divisheni ya kwanza baada ya kuvuna ushindi nyumbani dhidi ya Kisumu Hotstars.
Wanasuperstars waliwahi ushindi huo wa bao moja bila jawabu na kuandikisha alama tatu muhimu zilizowapaisha hadi nafasi ya kumi na moja kwenye jedwali kwa alama 24.
Kwa mujibu wa mkufunzi wa Superstars Frankline Musumba, wachezaji wake walijitoa kwa bidii kubwa hasa msimu ulipoanza kuporomoka kwao na kufikia nafasi ya kumi na tano.
“Nawashukuru mno wachezaji Wangu pamoja na mashabiki ambao wamesimama kidete na timu hii yetu ya Bungoma kwani ushirikiano wao pamoja na wachezaji na kikosi cha kiufundi umetuwezesha mno kujikwamua kutoka kule chini,” Musumba aliongezea.
Hadi kufikia sasa, Superstars imekamilisha michuano yote ya msimu huo ikiwa imetesa nyasi mara 28 huku wakivuna ushindi mara sita kutoa sare mara sita na kupoteza mara kumi na sita.
Ushindi huo wa sita unawakilisha asilimia 21.5 ya mitanange yote msimu huu huku sare hizo sita pia zikiwakilisha asilimia 21.5 navyo vipigo 16 vikiwakilisha asilimia 57. Aidha, Superstars wamecheza mechi 28 na kuandikisha rekodi ya kutopoteza kwa asilimia 43 huku wakipoteza kwa asilimia 57.
Vijana hao walifanikiwa kucheka na wavu mara 30 huku wao wakiruhusu takriban mabao 16 kutinga ndani ya wavu wao yakiwasazia mabao 14 pekee msimu huu.
Kwingineko ni kwamba kikosi hicho kimekuwa na rekodi nzuri nyumbani kwani kwa mechi 14 za nyumbani vijana hao wamekuwa na asilimia 0.79 ya mabao huku wakirekodi asilimia 0.36 ugenini.
Aidha, wenzao Nyota FC walijikakamua na kumaliza katika nafasi ya sita kwa alama 41 wakiwa wamesakata ngozi mara 27 wakiwahi ushindi mara 12 kutoa sare mara 5 na kubamizwa mara 5 pekee msimu huu.

Ushindi mara 12 kwa kikosi cha Nyota unawakilisha asilimia 44.4 ya michuano yote huku sare 5 zikisimamia asilimia 18.5 navyo vipigo 10 vikiwakilisha asilimia 37.1 msimu huu.
Kwa mujibu wa mkufunzi wa Nyota Ibrahim Shikanda, msimu huu umejaa ushindani bomba ila vijana wake walijituma kwa kadri ya vipaji vyao na kuvuna matokeo hayo hivyo basi kikosi hicho kinatazamia msimu ujao.
Source:KNA